RAIS MWINYI AVITAKA VIKOSI VYA SMZ KUENDELEZA UADILIFU



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali
Mwinyi amevinasihi vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza
uadilifu na uwajibikaji wa majukumu yao ya kila siku.
Dk. Mwinyi ambae ni Kamanda Mkuu wa Idara Maalum ya vikosi vya SMZ, alitoa
nasaha hizo viwanja vya JKU – Kama, alipozungumza na wapiganaji kwa lengo la
kuwapongeza kutokana na juhudi zao za kuhakikisha amani na utulivu nchini
vinaendelea kuimarishwa.
Alivitaka vikosi hivyo kuweka mbele maslahi ya nchi kwanza, uwajibikaji pamoja
na kusimamia uadilifu jeshini.
Rais Dk. Mwinyi alivisisitiza vikosi hivyo juu ya suala zima la kusimamia nidhamu
kwenye maeneo yao ya kazi ili kufanya kazi zao kwa uadilifu.
“Jeshi ni nidhamu ikikosekana nidhamu katika jeshi basi hapo hakuna jeshi”
alikazia Rais Dk. Mwinyi.
Dk. Mwinyi pia, alivipongeza vikosi hivyo kwa jitihada zao za kutoa huduma bora
kwa jamii wakiwemo Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) kupitia
hospitali yao iliopo Bububu pamoja na hospitali ya JKU, Saateni kwa huduma za
afya wanazozitoa kwa wananchi na nyengine za jamii vikiwemo vyuo vya amali na
taaluma.
Alivitaka vikosi hivyo kuwa mfano mzuri wa kutoa huduma bora kwa raia hasa
kwenye vituo vyao vya afya na taaluma vinavyohudumia jamii.
Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi aliwaagiza wakuu wa vikosi hivyo kuendelea
kusimamia uwajibikaji ili kuwe na tofauti baina ya hospitali za jeshi na za raia ili
wananchi wapate huduma bora.
Pia, Dk. Mwinyi alivieleza vikosi hivyo kuwa vinajukumu la kutoa malezi bora kwa
vijana na kuhakisha wanatoa vijana wazalendo wenye uchungu wa nchi yao
watakaopigania maslahi ya taifa lao.
Akizungumzia suala la kuwajengea uwezo maofisa na wapiganaji wa vikosi hivyo,
Rais Dk. Mwinyi aliwataka wakuu wa vikosi hivyo kuwaongezea uwezo wa
kitaaluma maofisa hao kwa kuwapatia fursa za mafuzo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Idara Maalum ya vikosi vya SMZ,
Masoud Ali Muhammed alisema, Idara Maalum ya vikosi vya SMZ zote tano
zikotayari kuendeleza jukumu mama la kuimarisha na kuendeleza amani, utulivu
na mshikamano uliopo nchini vinaendelea kusimama wakati taifa likiendeleza
maendeleo ya watu wake.
Alisema, Idara hizo pia zitaendelea kutekeleza maagizo, maono, mipango na fikra
za Kamanda Mkuu kwa utii wa hali ya juu.
Akiwasilisha risala ya vikosi vitano vya Idara Maalum ya SMZ, Katibu Mkuu wa
Idara hiyo, Issa Mahafoudh Haji alisifu juhudi kubwa ya Kamanda Mkuu wa Idara
Maalum ya vikosi vya SMZ, kwa aliyoyafanya kwa vikosi hivyo kwenye ujenzi wa
miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Pia, alieleza ushiriki wao kwenye miradi hiyo, umetanua uwezo wao wa ufahamu
na ujuzi wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku pamoja na kusifu hatua ya
kuwapandishia mishahara makamanda na wapiganaji kufuatia nyongeza ya
mishahara aliyoitoa kwa watumishi wa umma wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vinaundwa na Jeshi la kujenga
Uchumi (JKU), (KMKM), Kikosi cha Zimamoto na Uokozi, Valantia (KVZ) na Chuo
cha Mafunzo.
Imetolewa na IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

Comments